Friday, August 31, 2012

Mambo 10 yanayozuia mafaniko ya kimasomo



UMASIKINI

Umasikini ni kikwazo kikubwa cha mafanikio ya wanafunzi kimasomo, lakini tunashauri kwamba kila mwanafunzi anayetoka katika familia masikini ajitambue na awe tayari kuishi sawa na kipato cha familia yake wakati akitafuta elimu.

Ni muhimu kwake kubana matumizi na asiwe mtu wa kujihukumu kwa kukosa hili na lile, awe mvumilivu na mwenye kuomba msaada kila sehemu anayoona hawezi kuivuka kwa nguvu zake. Uaminifu, bidii na utii unaweza kumsaidia kuvuka kikwazo hiki.

Kuhusu suala ya kufukuzwa shule kwa kukosa ada ni vema kwa mwanafunzi mwenye kipato kidogo akawasiliana na mwalimu wake au viongozi wa serikali ili wamsaidie kutatua tatizo. Haifai kujifungia chumbani na kuanza kulia au kuamua kuacha shule kwa kukosa mahitaji. Mambo yote yanawezekana kinachotakiwa ni nia, mipango na uvumilivu.


MAPENZI

Kama kuna mtu hafahamu nini maana ya mapenzi basi kuanzia leo ajue kuwa mapenzi ni ulevi kama vilevi vingine. Mtu anayependa hulewa na kujikuta anaharibu ufahamu wake kama mtu aliyelewa pombe.

Walevi wa mapenzi huweza kufanya mapenzi hata barabarani sehemu ya wazi, huku akili zao zikiwapa taarifa kwamba watu hawawaoni, mambo ya aina hii hufanywa pia na walevi wa pombe.

Lakini ulevi wa mapenzi una nguvu kubwa ya kuiteka akili na kumtia mtu mshawasho kiasi cha kuacha kazi muhimu na kukimbilia kufanya ngono.

Hivyo, mwanafunzi ambaye anataka mafanikio ya kimasomo lazima aweke kando masuala ya mapenzi kwa lengo la kutoitwika akili mzigo ambao kwa umri wa wanafunzi wengi hasa wa kike ambao ni waitikiaji wa kauli za wavulana ni vigumu kwao kuhimili.

Licha ya baadhi ya watalaamu wa masuala ya afya kubainisha faida za kufanya mapenzi kwa afya ya mwili, bado uchunguzi unaonyesha kuwa wanafunzi wengi ambao wengi wao huwa katika umri mdogo hushindwa kuzuia hisia za mapenzi na kujikuta wanakuwa watumwa wa ngono.

Mapenzi kwa mwanafunzi yana hasara za aina mbili. Kwanza, mapenzi yanapokuwa moto huteka hisia na kumfanya msomi atumie muda mwingi kuwaza juu ya mahaba na hivyo kuufanya ubongo uone kuwa mapenzi ni kitu muhimu na hivyo kujituma kuhifadhi mambo ya mapenzi kuliko masomo.

Jambo la pili ni machungu ya mapenzi hasa yanapokuwepo mafarakano, mfano kuachwa, kusalitiwa, kuudhiwa, kugombana na migogoro yote ya kimapenzi huleta msongo wa mawazo na kumfanya mwanafunzi asiweze kusoma kwa kiwango stahili. Hivyo, inashauriwa kuwa mwanafunzi asijihusishe kabisa na mapenzi.

MIGOGORO YA KIFAMILIA

Kizuizi kingine cha kufanikiwa kimasomo kwa mwanafunzi ni kuwepo katika familia zenye migogoro. Baba na mama hawaelewani, ndugu wanagombania mali na kadhalika. Lakini inashauriwa kuwa mwanafunzi anayetoka katika familia za aina hii hatakiwi kujiingiza katika misuguano ya kifamilia.

Anachotakiwa yeye ni kuwaza juu ya masomo na kutupilia mbali mawazo yote yanayochipuka kuisumbua akili kuhusu mambo makubwa ya kiukoo. Kimsingi ufahamu wa mtoto hasa wa madarasa ya chini ni mdogo, hivyo hawezi kutatua mambo ya wazazi na akijaribu atakuwa anajisumbua na kujiweka katika matatizo makubwa zaidi.

Jambo muhimu kwake katika ngazi ya maisha yake ya shule ni kusoma na kama atakuwa na kitu cha kulilia ni mahitaji ya shule tu, na akiona migogoro hiyo inaathiri masomo yake, labda ada hazilipwi anachotakiwa kufanya ni kuwaeleza wazazi na ndugu wamsaidie kuhusu haki yake ya kupewa elimu na akishindwa katika ngazi hiyo awasiliane na viongozi wa serikali kwa ngazi yake ili wamsaidie.

KUFIWA NA WAZAZI/WALEZI

Uchunguzi unaonesha kuwa watoto wengi hushuka kimasomo baada ya wazazi au walezi wao kufariki. Hapa kuna mambo mawili, kwanza ni huzuni na pili kukosa upendo toka kwa walezi wao wapya.

Kuhusu huzuni mwanafunzi aliyefiwa na wazazi anashauriwa kuacha kabisa kuishi na wazazi wake waliokufa kwenye akili, haitakiwi muda wote kuwaza jinsi wazazi walivyokuwa wakimfanyia mema katika maisha. Wanasaikolojia wanasema hakuna jambo baya la asili isipokuwa mawazo ya mtu mwenyewe.

Ieleweke kuwa jinsi mtu anavyowaza ndivyo anavyojiumiza, huku ukweli ukibaki kuwa hawezi kuwarudisha wazazi wake duniani. Hivyo basi kila wakati mwanafunzi ambaye ni yatima anapoingiwa na mawazo ya kuwakumbuka wazazi anatakiwa kuyaacha kwa kuzungumza na wenzake, kucheza au kutazama sinema za kufurahisha. Si busara kutazama picha za wazazi enzi za uhai wao na kupendelea kuwazungumzia kila mara.

MALEZI YA BUGHUDHA

Baadhi ya watoto ambao wanalelewa na ndugu au walezi ambao si wazazi hukumbwa na kadhia ya kubughudhiwa kwa matusi na maneno ya masimango, kupangiwa kazi ngumu na kunyimwa muda wa kujisomea. Usumbufu huu wa kimalenzi upo hata kwa baadhi ya wazazi ambao wanakasumba za kubagua watoto.

Lakini ushauri unaotolewa hapa ni kwamba maisha siku zote hayana njia ya mkato na watafiti wa masuala ya maisha wanasema misukosuko ya kimaisha ina faida kwa watu wenye uelewa. Wakomonisti wanasema huwezi kutambua uwezo wa nahodha kwenye bahari iliyotulia bali kwenye dhoruba kali.

Ni wazi kuwa mwanafunzi anayesumbuliwa kwa bughudha ana nafasi kubwa ya kushinda masomo kama atazichukua kadhia hizo kama changamoto za kumfanya asilale na kujitambua kuwa yuko kwenye bahari chafu isiyo salama.

Ukiwa kwenye familia za aina hii, soma kwa bidii, usijihukumu sana, jishushe na uwe tayari kutumia unachopewa bila kunung’unika, usijibu mapigo kwa ugomvi au kufokeana na wakubwa wanao kulea. Uwe tayari kutumika kama mtumwa ili baadaye uishi kama mfalme. Ila kama mambo yatazidi pendelea kushauriana na wazee wa ukoo au majirani ili wakutanue mawazo.

STAREHE

Maisha ya shule yanakata nidhamu ya matumizi ya pesa, muda na sheria za shule. Mwanafunzi hawezi kufanikiwa kimasomo kama ataendekeza mambo ta starehe, mfano kwenda disko, kukesha baa na kushiriki mapenzi na wanawake/wanaume kwenye majumba ya anasa.

Haishauriwi mwanafunzi kuwa mtu wa starehe kwani ni rahisi sana kwake kupata matatizo ambayo yanaweza kumharibia masomo yake, mfano kupigwa na kuumizwa, kukamatwa na polisi na kuhusishwa na matukio ya uhalifu na hata kukosa muda wa kuupumzisha mwili na akili.

UFUNDISHAJI DUNI

Walimu wasiokuwa na sifa za kufundisha ni tatizo kwa mafanikio ya mwanafunzi kimasomo, lakini wakati huo huo uhaba wa walimu nao huchangia kushusha kiwango cha kufaulu. Inashauriwa kuwa wanafunzi ambao hawafundishwi vizuri wamuone mwalimu wao wa taaluma na kumueleza tatizo lao ili ufumbuzi upatikane.

Lakini wakati huo huo ni sahihi kuwasiliana na wazazi/walezi na kuwataarifu uhaba wa walimu kwenye shule yako na kuwataka wakusaidie. Inaposhindikana kwa ngazi ya familia ni vema viongozi wa kitaifa wakajulishwa na hatua za kuhama shule zinaweza kufikiwa endapo kikwazo hiki kitakosa ufumbuzi.

UKOSEFU WA VIFAA

Shule nyingi zimekuwa hazina vifaa vya kutosha, hili nalo ni tatizo kubwa na dawa yake ni kwa wazazi wanaojiweza kuhakikisha kuwa wanawanunulia watoto wao vifaa binafsi vya kujisomea. Wakati huo huo ni wajibu kwa wanafunzi wa shule mbalimbali kuwa na utamaduni wa kubadilisha vitendea kazi ili kupata unafuu wa tatizo hili.


KUHAMISHWA SHULE

Mwanafunzi anapohamishwa shule anaweza kuathirika kisaikolojia, lakini kama imebidi ni vema akatumia vidokezo nilivyoeleza huko nyuma katika kupata uenyeji na kuzoea mazingira mapya.

Haipaswi kuhuzunikia marafiki na walimu alioachana nao na kusahau kuwa yeye anajukumu la kusoma kwa bidii na kupata matokeo mazuri.

UDHALILI

Kuna wanafunzi ambao wanashindwa kufanikiwa kimasomo kwa sababu wanajiona wao ni duni mbele ya wenzao katika mavazi, uwezo wa kifedha na kadhalika. Kwao linakuwa ni jambo ngumu kujieleza mbele ya wenzao na muda wote hujawa na aibu na hali ya kutojiamini.

Kasoro hii ni kubwa na huwakwamisha wengi katika kupata uelewa wa mambo. Ni wajibu wa mwanafunzi kujiamini na kutupilia mbali aibu na kueleza hisia na kile anachofahamu mbele ya mwalimu na wanafunzi wenzake bila kujali kama atakosea au atachekwa. Mwanafunzi anatakiwa kuwa na mazoea ya kubadilishana mawazo na wengine na kuacha kujitenga.

Tabia hii si nzuri, mwanafunzi ambaye anataka kuwa na kumbukumbu juu ya yale aliyojifunza lazima awe tayari kushirikiana na wenzake katika kusoma, kujadiliana na kusaidia.

Labels: ,

1 Comments:

At February 13, 2013 at 4:39 AM , Anonymous Anonymous said...

N i kweli kabisa ulicho kionge hamna palipo kosewa

 

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home