Monday, August 13, 2012

Ukitaka furaha, gharamia kwanza furaha ya mwenzi wako


                                                                              


SANAA ya busara katika maisha inajumuisha vitu vinne: Nia na malengo, Mungu ana nafasi yake, hatua chanya na mafanikio endelevu. Ukikaribisha busara kama kanuni yako ya kuishi, maana yake unahitaji amani na furaha.

Ukitaka kuishi kwa busara ni lazima uwe na mtazamo wenye furaha. Lazima uingalie dunia kwa fikra na macho, angalia jinsi watu wengine wanavyosononeka kwa kuikosa, halafu chukua mfano wa wanaoshi kwa amani yenye afya.

Unapoitazama dunia kwa fikra, hapo unapaswa kubeba ufahamu wa uchafu mgumu uliopo. Fikra zinakuja kutokana na kumbukumbu ambazo hutafsiri uzoefu wa nyuma ambao utakupa mwanga wa hali ya sasa. Hatua hizo zinatakiwa kutoa muongozo katika kuandaa furaha.

Mwandishi wa saikolojia, Swami Sukhabodhanda katika makala yake yenye kichwa “Love and Happiness: Art of Wise Living Brings Great Joy” ameandika:

“Mtu sahihi ni yule anayejifunza kupunguza msongo wa mawazo, Anayejifunza kuongeza furaha na kupanua uwezo wake.”
Hii ina maana kuwa kutafuta furaha ni wajibu wako, lakini swali la kujiuliza ni hili, mwenzi wako akiwa hana amani wewe utaipata wapi? Akiwa amekasirika utaweza kucheka? Jibu ni kwamba haiwezekani na endapo moyo wako una amani wakati mwenzako amejikunja, ni wazi kwamba penzi lenu limejaa mashaka.

Hivyo basi, naungana na Swami kushauri kwamba ni lazima kila mtu ajifunze kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza furaha. Ukifanikiwa kuiweka chanya furaha ya mwenzi wako na yako itapatikana. Zingatia msemo kuwa ninyi ni kitu kimoja wewe ni yeye!

Watu wengi wamekuwa wakishindwa kustawisha uhusiano wao kwa sababu wanashindwa kuishi ndani ya wenzao. Wanatenda mambo ambayo yanawaumiza wenzi wao bila kujiuliza. Hawana malengo chanya!

Mtu mwenye malengo mazuri katika mapenzi ni yule ambaye anajiuliza kabla ya kuzungumza au kutenda. Anatafakari kauli au kitendo na matokeo yake. Pointi kuu ni mapokeo ya mwenzi wake. Ni kosa kufanya tukio lolote au kutoa matamshi yanayoweza kumuudhi mwenzako.

Ni lazima uwe na angalizo kwamba kwako linaweza kuwa dogo lakini kwa mwenzako ni kubwa. Heshimu kosa lolote kwamba linaweza kuhatarisha uhusiano wako, kwa hiyo jichunge kila eneo.

Wewe ni mtu tu duniani, inawezekana uzito wako ni mdogo. Ukiwepo na usiwepo taifa halisomi upungufu wowote! Hata hivyo, kupitia mapenzi wewe ni dunia mbele ya mwenzi wako. Kila kitu hakina thamani kwake bila uwepo wake, kwa hiyo heshimu hisia zake, ingia gharama kumletea furaha.

Nimeeleza hapo juu kuwa mfumo sahihi wa mapenzi ni kuishi ndani ya mwenzake. Yaani kuzijulia hisia zake na kujenga nidhamu ya kuepuka kumpa maumivu yasiyo na sababu. Unaelewa kuwa mwenzako hapendi uchelewe kurudi nyumbani, kwa hiyo usifanye makusudi kuchelewa mitaani.

Ni kweli unapenda kuketi na wafanyakazi wenzako au marafiki mkipata za moto na baridi baada ya kazi. Lakini wakati unatekeleza hilo, kwa kila hatua jiulize, je, hicho ndicho ambacho mwenzi wako anakihitaji? Kama ndiyo basi fanya, ikiwa jibu ni kinyume chake, changamsha miguu umuwahi nyumbani.

Jiulize swali; Kuna sababu gani ya kugandana na marafiki mitaani wakati mwenzako amenuna nyumbani? Jiongeze lingine; Mtakapokuwa ‘mnaparurana’ nyumbani hao unaowaendekeza watakuwepo? Pengine wakati wao wanalala usingizi mzuri, wewe kwako hakulaliki.

Tafakari; Kuna mambo mengi ambayo mnachangia pamoja, ulimwengu ambao unapita naye ni usiku wa giza kwa wengine. Hulioni kama hilo ni maalum? Tambua thamani ya mwenzi wako, hivyo tekeleza furaha yake na umtimizie kwa vipimo sahihi.

Furaha ya mpenzi wako ni gharama, kwa hiyo unahitaji kujipanga ili kumtimizia. Katika uhusiano wa kimapenzi, hauna cha kupoteza kwa kugharamia amani na furaha ya mpenzi wako. Umegundua kwamba ili mwenzio awe sawa ni lazima uende Zanzibar, uwezo upo fanya hivyo!

Tafsiri yake ni kuwa unatakiwa kufanya kila linalowezekana ili mpenzi wako awe na furaha. Sifa ya ubabe na kupuuza hisia za mwenzi wako haina maana. Ukimpuuza leo, maana yake unataka kesho akupuuze. Akikutenda wewe utafurahi? Usingoje msemo wa mkuki kwa nguruwe ukufike!

Zipo hasara nyingi ambazo unaweza kukutana nazo endapo utashindwa kugharamia furaha ya mwenzi wako. Hii inamaana kuwa ni vema unisome vizuri ili ujifunze.

Asilimia kubwa ya watu ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi, husumbuliwa na tatizo la kutotengeneza penzi. Wakiongozwa na msemo kuwa kila kitu hupangwa na Mungu, nao huacha mapenzi yao yaende kama yalivyo. Hawaamini kuwa barabara ilichongwa, ndiyo magari yakapita.

Ukiona vyaelea ujue vimeundwa! Hii inamaana kuwa kila kinachostawi, nyuma yake kuna ujenzi uliofanyika. Usimuone babu na bibi wanasherehekea miaka 50 ya ndoa yao ukadhani ni jambo lililokuja lenyewe. Kuna mambo ya msingi ambayo waliyafanya kuhakikisha wanadumu mpaka kuzikana.

Ukiwa mwingi wa hasira, matatizo yanayotokea hutaki kuyaweka mezani ili myajadili na kuyamaliza, kila siku utakuwa unabadili uhusiano. La! Hutabadili lakini utabaki kwenye penzi ambalo unaishi bila amani. Huna furaha! Ni mpenzi lakini hamfungamani, mnakuwa kama wapinzani wa jadi!

Uhusiano bora ni ule ambao wanaoujenga ni watu makini na ambao wanajua nini ambacho wanakifanya. Wenye kufahamu thamani ya penzi lao kila mmoja anaheshimu umuhimu wa mwenzake. Wanaoguswa kutoa chochote kuhakikisha wanaendelea kuwa bora kimapenzi.

Hii ndiyo sababu ya kukutaka uhangaike na ikiwezekana utumie gharama yoyote ili mwenzi wako awe na furaha. Utengeneze thamani yako kwake, kiasi kwamba akikuona aone mbele yake kasimama mtu aliyeishikilia dunia yake. Inawezekana! Mapenzi ni ujanja, utundu, kuguswa na kujitolea!

Huna sababu ya kushindwa kugharamia furaha ya mwenzi wako kwa sababu ukiacha gharama yake ni kubwa. Utakosa kila kitu muhimu ambacho mtu sahihi angependa kupata kutoka kwa mwenzi wake. Na hiyo itakusumbua! Kama hutafikiria, basi utaona kwa wengine na utatamani!

Hapa chini nakuchambulia hasara ambazo unaweza kukutana nazo kwa kushindwa kuhudumia furaha ya mwenzi wako;

UTAKOSA AMANI
Misongo (stresses) ya kimaisha inatesa. Inawezekana unafanya kazi sana. Wakati mwingine masuala ya kiofisi au biashara hayaendi kama inavyotakiwa. Unashinda siku nzima ukipigana kuhakikisha unaendelea mbele. Iwe umeajiriwa, umejiajiri au umeajiri! Kichwa hakitulii mpaka unahisi ni kizito.

Kufikia hapo, bila shaka unahitaji faraja. Ni kipindi ambacho huhitaji mwenzi sahihi ili aweze kukusahaulisha matatizo ya kimaisha. Mtu ambaye anakujua ulivyo, kwa hiyo inamuwia rahisi kutambua kwamba upo kwenye matatizo na kuchukua hatua zinazofaa kurekebisha hali.

Fikiria kwamba ukiwa katika hali hiyo, unarudi nyumbani ambako unakutana na moto mwingine. Amani hakuna! Kichwa chako kinaweza kuchanganyikiwa. Kama sivyo, maradhi ya moyo yatakunyemelea. Kupata kilicho bora, kiandae. Lima shamba na kupalilia ili upate mavuno mazuri.

Ukifanikiwa kumuweka mwenzi wako katika hali ya furaha, utapata faraja muda wote. Yakikufika, ukirejea nyumbani utakuta amani. Utakutana na tiba ya msongo wa mawazo ulionao. Hiyo ndiyo tafsiri ya upendo, kwa hiyo usije kukosa utulivu wa moyo. Anza leo kumfurahisha ili naye akupe mahaba tele!

UTACHOKWA HARAKA
Hakuna kitu kibaya kwenye mapenzi kama mtu kuchokwa na mwenzi wake. Lakini hilo siyo zito, ni rahisi mno kama hutoamua kushughulikia kasoro ulizonazo.

Huna ubunifu, mwenzi wako haoni kitu chochote kipya. Mwenzi wako hana furaha wewe hujishughulishi. Ataanza kukuona ni mzigo na mwisho atakuchoka. Usikubali hali hiyo ikutokee, anza leo! Maisha ya kimapenzi ni mazuri sana endapo utaamua.

MTASHINDWA KUJADILIANA
Mwenzi wako hana furaha, wewe unaingia mlango huu naye anapitia ule. Hayo ni maisha mabaya mno! Mnapatwa na mambo ambayo mngependa kushauriana, lakini mnashindwa kufanya hivyo kwa sababu mnaishi kama Simba na Yanga.

Kuna watu wanaishi kwa kalamu, wanalala mzungu wa nne! Kama matumizi, yanawekwa mezani, akitaka kutoa agizo anaandika ‘kimemo’ na kukiacha juu ya stuli! Hawaguswi kutafuta furaha yao, hawataki kuzungumza na kumaliza tofauti zao.

Matokeo yake ni siri za ndani kuzagaa mitaani. Hili likikufika ni sawa na msiba. Chukua hatua!

HUTAPATA HUDUMA BORA
Mwenzi wako anahitaji kuwa na furaha ili aweze kukupa huduma bora. Amini kwamba mwenzi wako ndiye ambaye anaweza kukufanya hii dunia uione yote ni yako. Changamka leo!

Unahitaji huduma bora kutoka kwa mwenzi wako, na hilo anaweza kulitimiza endapo atakuwa na furaha dhidi yako. Hii inamaana kwamba kuanzia sasa, punguza maudhi kwa mwenzi wako na umzidishie amani. Akupende na aamini ndani ya nafsi yake kwamba wewe ndiye mtu bora zaidi maishani mwake.

Ukimfurahisha, atakupa huduma bora ambayo huwezi kuipata popote. Bila shaka atakapokuhudumia, nawe utajiona umepata mwenzi sahihi wa maisha yako. Hayo ndiyo mapenzi. Yakistawishwa hustawi!

Labels: ,

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home