Rungu la Dk Mwakyembe latua kwa meneja Tazara
WAZIRI wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema atamtimua kazi Meneja Mkuu wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), Abdallah Shekimweri, iwapo atashindwa kusimamia majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuwapa vitendea kazi na posho wafanyakazi wa shirika hilo.
Rungu la waziri huyo lilianza Juni 5, mwaka huu baada ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi na kumteua rubani wa muda mrefu, Kapteni Lusajo Lazaro kukaimu nafasi hiyo.
Mbali na uteuzi huo pia alitangaza kuwasimamisha kazi vigogo wengine wanne wa shirika hilo ambapo baada ya siku chache alianika ufisadi unaodaiwa kufanywa na kigogo huyo.
Lakini jana wakati akiwa katika ziara yake ya kushtukiza katika karakana za Tazara, Dk Mwakyembe alisema kuwa haridhishwi na utendaji kazi wa Shekimweri.
Mbali na kutembelea Tazara, pia alifanya ziara bandarini na katika ofisi za Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Akiwa katika ziara hiyo aliahidi kukutana na uongozi mzima wa Tazara ili kujadili matatizo yaliyopo katika shirika hilo ikiwa ni pamoja na ubovu wa reli, lengo likiwa ni kuyapatia ufumbuzi.
Mmoja wa wasaidizi wake ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini licha ya kuwa alikuwa amembatana na waziri huyo katika ziara hiyo alisema kuwa suala la kumtimua kazi Shekimweri siyo jambo la utani.
“Dk Mwakyembe ameshatuma barua kwa uongozi wa Tazara nchini Zambia, amewaeleza wazi kuwa haridhishwi na utendaji kazi wa (Shekimweri) na yupo tayari kutoa uamuzi, itakuwa kabla ya Oktoba mwaka huu,” alisema msaidizi huyo na kuongeza;
“Si unajua hili shirika linaendeshwa kwa ubia wa Tanzania na Zambia, hivyo kama unataka kuchukua uamuzi ni lazima upande mwingine uwe na taarifa.”
Dk Mwakyembe alisema haridhishwi na ufanyaji kazi unavyoendelea katika Karakana ya Tazara na kumtaka Shekimweri kuwapa vifaa wafanyakazi hao na iwapo atashindwa kufanya hivyo atalazimika kumfukuza kazi. “Tutafukuzana hapa, watu wapo tayari kufanya kazi ila wanakwamishwa, mwambieni Shekimweri kuwa nitamfukuza kazi na nitarudi tena Jumatatu (kesho),” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kuwa ni jambo la ajabu kwa menejimenti ya Tazara kushindwa kutoa fedha kwa watumishi wake wakati Serikali imeshatoa fedha za ukarabati wa mabehewa ya treni yanayotakiwa kuanza kutoa huduma ya usafiri kuanzia Oktoba mwaka huu.
Dk Mwakyembe alihoji sababu ya menejimenti hiyo kukalia fedha hizo wakati zinapaswa kulipwa kwa wafanyakazi hao wanaoendelea kukimbizana na muda ili kumaliza ukarabati huo. “Fedha mnaziweka makao makuu kwani ni maua hayo? Walipeni watu fedha zao na mnunue vifaa, tutafukuzana hapa na hakuna wa kunilaumu,” alisema Dk Mwakyembe.
Aliitaka menejimenti ya Tazara kukamilisha ukarabati wa mabehewa 14 ambayo aliagiza yafanyiwe ukarabati kwa kuwa mpaka sasa ni mabehewa manne tu ndiyo yanayoonekana kukarabatiwa.
Baadhi ya wafanyakazi waliokuwapo katika maeneo yao ya kazi walimweleza, Dk Mwakyembe kwamba shirika hilo haliwawekei fedha zao za mifuko ya hifadhi ya jamii, suala ambalo waziri huyo aliahidi kulifuatilia kwa ukaribu.
Akiwa katika Karakana ya TRL, Dk Mwakyembe aliridhishwa na utendaji kazi na kusema kuwa mpaka Oktoba mwaka huu treni ya Reli ya Kati itaanza kutoa huduma zake kama ilivyotangazwa.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe alisema mashine ya kushusha na kupakia mizigo katika meli karibu itafungwa kwa kuwa ujenzi wa reli kwa ajili ya kusimamisha mashine hiyo unaendelea vizuri.
source: Mwananchi, Jumapili.
Labels: ~ Siasa ~, news updates
0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home