Mh. John Mnyika, mbunge wa Ubungo.
Kauli ya awali kufuatia madai ya kizushi na kijinga ya CCM kuwa CHADEMA imepewa mabilioni na nchi za nje
Katika mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM
kutoa madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa habari
kuhusu CHADEMA baada ya CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na mipango
yake ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’
katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali
nchini. Nitatoa tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada ya kupata
taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai yaliyokwisha
sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM nachukua fursa hii kutoa
kauli ya awali kama ifuatavyo:
Kuibuka huku kwa CCM na kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM
inaumizwa na namna ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA
kwa hali na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la
mabadiliko kwa kutumia siasa chafu. Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya
Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina
baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai
yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven
Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa
mbinu mbalimbali.
CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha
haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi
waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha za chafu kifisadi kama
zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine
vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa zilizofanywa na CCM kwa
nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka
vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha tamaa umma wa watanzania
unaochangia vuguvugu la mabadiliko.
Viongozi wa CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na
kujaribu kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu
wachache wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote
wakati wote; na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi
kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.
Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi
kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara
ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango
kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote
kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko ya kweli.
Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi
kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena
kuitaka CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje
ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya shilingi katika
siku za karibuni au inatarajia kupokea.
Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha
ya vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao
wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa
kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta,
gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.
CCM ilipaswa ieleze watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua
magamba ya ufisadi kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya
msukumo wa CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi
hao ni pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba
mibovu.
Ikumbukwe kwamba madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa
na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada
ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka
mataifa ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM
madarakani.
Itakumbukwa kwamba wakati huo nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza
kusudio la kumchukulia hatua zaidi na kwa upande mwingine niliyataka
mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba
mataifa hayo yalikanusha madai hayo ya CCM na Sophia Simba mwenyewe
alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.
Nimeelezwa kuwa CCM imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa
mabilioni toka nje kwa kuwa nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi
na kudai kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiweka nchi rehani.
Madai haya yaliwahi kutolewa pia na Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi
Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe kutaja
nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote
wa CCM na Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea
mabilioni kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.
CCM inatoa madai hayo kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi
bora, sera makini, mikakati sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari
wa mbele katika kutetea rasilimali za taifa na watanzania kutambua
kwamba taifa letu litaepushwa kutumbukia kwenye laana ya rasilimali kwa
kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na
kuichagua CHADEMA.
CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea fedha kutoka nje
kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu na mataifa ya nje
pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya uporaji wa rasilimali
za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha ya mafisadi kwa
kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba ya madini na
tutaendelea kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na gesi ambayo
tayari vigogo wa Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza kuingia
mikataba mibovu na kuingiziwa fedha katika akaunti zao za nje ya nchi.
Hivyo, badala ya CCM kutoa madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia
mikataba na serikali au makampuni ya nje, CCM ieleze watanzania
imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya viongozi na wanachama wake
waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali muhimu nchini ikiwemo
madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa letu na kutoa
mikataba hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya
mabadiliko ya kweli.
Hivi karibuni Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema
kwamba serikali inayoongozwa na CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya
ya ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi
watanzania kwa ufisadi uliofanyika kwenye madini na rasilimali nyingine
na kuishukuru CHADEMA kwa kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote
kusimamia mabadiliko ya kweli.
CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba inayoihusu CHADEMA ingetoa
mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza Serikali kudai CHADEMA
kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo kinyume cha sheria bila
vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri wazi kuwa chama
legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi na badala
yake kimejikita katika propaganda chafu.
CHADEMA tangu kuanzishwa kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano
(MOU) bila masharti yoyote na vyama rafiki vya ndani ya Afrika na
duniani na makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni
sehemu ya CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi kuhusisha
wala hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa
ajili ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM.
CHADEMA kimekuwa chama kiongozi kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango
cha matumizi yake ya fedha na vyanzo vya fedha husika huku kikitegemea
kwa kiwango kikubwa michango ya wanachama na wapenzi wa chama hapa
nchini pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku inayotolewa kwa vyama vya
siasa.
CCM imekuwa na kawaida ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine
yakiambatana na kutoa nyaraka za kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA.
Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai
ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa
mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA
toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya
uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo
alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali
kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi.
Hivi karibuni, CCM imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile
ilichodai kuwa ni maazimio ya kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya
walimu, madaktari na mipango mingine ya kuhujumu serikali; hata hivyo
waraka huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa kughushi.
Mikakati yote hiyo michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo
CHADEMA inaanza operesheni Sangara na mikakati mingine ya kuleta
mabadiliko nchini na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa
ambapo CHADEMA inaendelea na operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo
watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na
kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
source; mnyika.blogspot.com