Tuesday, July 24, 2012

NI NGUVU ZINAZO ONGOZA MAISHA


Mimi ni muumini wa nguvu za kimaumbile. Naamini kwamba kila kinachopandwa, hatimaye huvunwa kwa njia ile ile, kama leo hii mtu akitenda wema, ni wazi atavuna wema huo, iwe anataka au hataki. Kwa kawaida maisha yetu yanazingirwa na nguvu tunazopanda wenyewe ingawa hili limekuwa gumu kwetu kueleweka.

Naomba nikupe mfano wa watu ambao huenda unaweza kuwafahamu. Miaka mingi iliyopita, mkulima mmoja kule Uskochi, alikuwa akifanya kazi zake shambani. Ghafla alisikia kelele kutoka bondeni .

Mkulima huyo, bwana Fleming alikimbilia huko bondeni kuona kulikoni. Kufika huko, alikuta kuna kijana mmoja ambaye alikuwa anazama kwenye tope.

Kumbuka kwa wenzetu, kuna maeneo ambayo mtu anaweza kukanyaga na kujikuta akizama pole pole hadi kumezwa kabisa na tope na kufa. Mkulima huyu alijitahidi hadi akamwokoa kijana huyo.

Kwa kawaida wakulia wengi hawakuwa tayari kuhatarisha maisha yao, kuokoa mtu ambaye anazama. Kwanza, hadi mtu kufikia mtu kuzama shambani kwako maana yake ni kuwa aliingia eneo lako bila idhini. Lakini, kumwokoa mtu ingekuwa ni sawa na mtu anayeokoa kujiweka katika hatari ya kufa pia. Lakini mkulima huyu alijali zaidi utu wa yule aliyekuwa anaomba msaada.

Kesho yake asubuhi, mkulima yule alishangaa kuona mkokoteni wa farasi umefika nyumbani kwake. Mikokoteni hii ilikuwa ikimilikiwa na watu wenye uwezo au kutoka koo ya kifalme. Mgeni huyu alikuwa ameongozana na yule kijana aliyeokolewa. Mtu aliyekuwa na mkokoteni ule, ambao kwa sasa tungesema Benz ile, alijitambulisha.

Huyu alikuwa ni baba wa yule kijana aliyeokolewa na mkulima yule. Huyu mgeni aliuliza, 'wewe ndiye ndiye uliyemwokoa mwanangu jana? Ninashukuru sana kwa hilo. Nimekuja kukulipa kwa wema wako.' Mkulima Fleming alisema kwamba, hahitaji kulipwa chochote kwa kile alichofanya.

Wakati huo mtoto wa mkulima yule ambaye alikuwa makamu mamoja na kijana aliyeokolewa, alijitokeza kutoka ndani. Yule mgeni aliuliza, 'Huyu ni mwanao,' Yule mkulima alijibu kwa kujidai, akisema, 'ndiyo.' Yule mgeni alisema, 'naomba nimsomeshe kwa kadiri ambavyo ningemsomesha mwanangu.'

Halafu aliendelea, 'Kama ni mtoto ambaye atakuwa na moyo kama wa baba yake, basi atasaidia watu wengi sana na atafanya dunia kuwa mahali bora zaidi.' Mkulima alikubali ofa ile ya mwanae kusomeshwa. Kwa hiyo, kijana akawa amepata mfadhili mwenye fedha kumsomesha kutokana na wema wa baba yake.

Ni kweli, mgeni alimsomesha kijana huyu hadi kiwango cha juu kabisa cha elimu, kwenye shule bora kabisa za wakati ule. Kijana huyu alikuja kusomea udaktari kwenye chuo ambacho kilifahamika kama, St. Mary' Hospital Medical School, kilichopo London, Uingereza. Maana yake ni kwamba alikuwa ni Daktari.

Huyu kijana ni mtu maarufu sana hapa Duniani. Kwa nini? Ni kwa sababu, ndiye mtu aliyegundua dawa aina ya Penicillin. Huyu si mwingine, bali ni Sir Alexander Fleming.

Baada ta kumaliza masomo yake na kugundua dawa hiyo, kilitokea kisa kingine. Yule kijana aliyeokolewa kuzama topeni na yule mkulima, alipatwa na maradhi ya homa ya mapafu {Pneumonia}. Kilichookoa maisha yake kilikuwa ni dawa ya Penicillin ambayo iligunduliwa na mtu aliyesomeshwa na baba yake, katika kulipa shukrani ya msaada uliotolewa kwa mwanae.

Naomba nikwambie kwamba yule Tajiri hakuwa mwingine bali Lord Randolph Churchill, ambaye ni baba wa mtu aliyekuja kuwa maarufu sana duniani kwa uongozi na hekima yake, Sir Winston Churchill. Huyu bwana ndiye aliyeokolewa kule kwenye tope na kuja kuokolewa tena na Penicillin. Umeelewa?

Je, wakati mkulima yule anamwokoa kijana yule, bila masharti au kinyongo, alikuwa anategemea kupata kitu gani kutoka kwake au kwa baba yake, ambaye wala hakuwa akimjua? Hakuwa anategema chochote, bali alitenda wema tu. Tunapotenda wema huwa hatutarajii kulipwa.

Lakini tunapotenda wema, ni kwa namna gani tunaingia kwenye mfumo wa nguvu za kimaumbile? Naomba nitumie habari hii kukufahamisha. Kila jambo jema au baya tunalotenda linatuweka mahali ambapo tunaingia kwenye njia ya nguvu inayoendesha mambo ulimwenguni. Hatuna haja ya kuhangaika kujua, tumeingia katika nguvu gani, kwani tujue au tusijue, tutaingia tu.

Kwa mfano mkulima alimwokoa kijana, badala ya kusema , 'ngoja life, kwa nini hayasikii yakiambiwa yasiingie kwenye maeneo ya watu?' Kumwokoa kwake kulifanya baba wa kijana huyu kutaka kulipa fadhila. Mkulima alikataa malipo mengine yote, bali 'ofa' ya mwanae kusomeshwa . Kumbuka , mkulima kwa njaa yake angekubali hela haraka sana, lakini alikataa.

Kwa kukataa kuuza ule wema aliotenda kwa kijana akawa ameingia kwenye nguvu chanya zaidi. Kukataa huko kulizua tajiri kutaka kumsomesha mwanaye. Kama angekubali fedha, huenda mwanae asingekuja kusoma na kuwa daktari maarufu duniani na mgunduzi wa dawa iliyookoa maisha ya mamilioni ya watu.

Huyu tajiri, naye ameamua kulipa fadhila ambayo ni nguvu chanya. Pale mkulima alipokataa kupokea zawadi ya fedha, yule tajiri bado aliona atajisikia vizuri kumtendea jema mkulima. Alimwona kijana wake na akaona kumsomesha katika kiwango cha juu lingekuwa jambo ambalo lingempa ridhiko. Alifanya hivyo, na hiyo fadhila yake, ndiyo ambayo inakuja tena baadae kumwokoa mwanae.

Labels: ,

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home