Friday, July 27, 2012

*** Play gal - 54 ( Revenge)


Ilipoishia…

Nikiwa bado katika hali ya kuongea na dereva teksi na hata sikuwa nimepanda ile gari wala kupatana naye bei rasmi. Mara kwa ghafla akatokea mwanamama mnene mrefu kidogo. Alikuwa mweusi huku sura yake ikikunjamana vilivyo mithili ya mtu anapopigwa jua la utosi. Macho yake yalionesha kuwa tata kwani mbali na machozi yaliokuwa yakimtoka pia yalikuwa ni mekundu kama mtu aliyefiwa ama kumpoteza mume au mtoto wa kumzaa.
“..unakwenda wapi Malaya mkubwa wewe..?”
Aliuliza kwa sauti ya jazba. Sikuwa namtambua zaidi yakumtolea macho mimi pamoja na dereva teksi. Mwili wangu ulikuwa tayari umeshakata tamaa ya kuishi huku nikihisi kama kojo likiteleza ndani ya suruali yangu iliyokuwa imenibana…

Sasa endelea….
Uoga uliochanganyikana na kutetemeka mwili mzima ni kati ya vitu ambavyo vilikuwa bado vinasumbua halmashauri ya kichwa changu huku nikibaki njia panda nikiendelea kumkodolea macho yule Mmama alioonesha kunikazia macho vilivyo huku akiendelea kutoa matusi makubwa na mazito.
“...na leo ndio utanitambua vizuri..? yaani siku ya nne leo huonekani cha nyumbani wala hujui hata watoto wanaishije huko..? Wewe kazi kuendesha hiki ki teksii chako tena bila hata haya unaongea tu na wanawake shenzii kabisa wewe mwanaume..!”
Nilishusha pumzi huku nikinyanyua mkono wangu wa kulia nakushika kifua changu huku nikijihisi mapigo yangu ya moyo yalivyokuwa yakiendelea kunitoka. Nikatoa kitambaa nakuanza kujifuta futa jasho lilikokuwa limeshaanza kupenyeza kwenye uso wangu nakupitilizia shingoni. Kumbe yule dererva teksi niliokuwa naye ndio alikuwa akiongeleshwa na mke wake sijui. Aibu kubwa ikanijaa ghafla Tina mimi nakufikiri kuwa kumbe ningeumbuka kama ndio angekuwa mke wa mchungaji James.
“..Naona hapa tena hamna safari..?, embu ngoja nitafute usafiri mwingine…”
Niliondoka zangu nakuwaacha pale yule dereva teksi na mke wake wakiendelea kugombana. Nikatafuta teksi nyingine ambapo ilinifikisha mpaka stendi kubwa ya mabasi. Umati wa watu ulikuwa umefurika ndani ya stendi hii ya mabasi huku kila mmoja akiwa yuko ‘bize’ si kwa kubeba mizigo yake bali kwa purukushani za hapa na pale za kugombea tiketi. Nilijisogeza mpaka eneo la karibu na basi la ‘Mohammedi trans’ ambayo ni mabasi maarufu sana kwa safari ziiendazo dar es salaam.
“.. Nauli ya hapa mpaka dar shilingi ngapi..?”
“..nauli yake shilingi elfu  thelathini na nane tu..”
Nilichomoa hela kwenye suruali tena hela zenyewe zile nilizokuwa nimeziiba baada ya kufanya mauaji ya mchungaji James. Nikatoa shilingi elfu arobaini na kumpatia yule mkata tiketi.
“.. nipe tiketi moja..”
“..ya lini..? maana za leo mpaka kesho zote zimejaa…”
“..zimejaa..?”
“..ndio dada. Zimejaa na hapa unavyoona wanafunzi wengi wa vyuoni haswa wale wa chuo cha Mtakatifu Agustino na chuo cha biashara ndio wamefunga hivyo tangu juzi mabasi yanawabeba wao wanafunzi tu..”
“..Ooooh Mungu wangu..!! sasa nitafanyaje jamani na nahitajika Dar es salaamu leo leo hata niingie saa ngapi..?”
“..labda usubiri basi letu jingine linatokea Kigoma litapita hapa hivyo kaa pale usubiri..”
Kidogo akili yangu ikakaa sawa nakusogea mpaka eneo la kupumzikia abiria nakuanza kusubiri. Ilinichukuwa kama masaa mawili kusubiri huo usafiri wa kutokea Kigoma. Bado hakukuwa na dalili zozote wala hata taarifa zinazotia nguvu juu ya hilo basi litokalo huko kigoma. Jua kali lililochora kivuli kikubwa chini ilimaanisha dhahiri kuwa itakuwa tayari imetimu mchana tena ule mchana wakuanzia saa sita nakuendelea maana jua lilikuwa kali sana. Nilikiwa bado nimezubaa mwenyewe mara ghafla nikahisi kama kuna mtu ananigusa mgongoni taratibu. Sikutaka hata kugeuka kwani niliamini kwa asilimia zote huenda atakuwa ni mdudu ama kweli kuna mtu. Nilichukua mkono wangu wa kulia nakuanza kupapasa papasa kwa nia yakukitoa kitu kinachonigusa kwa begani. Kadri nilivyozidi kukitoa ndipo kilizidi kunibonyeza kwa nguvu na kwa sasa nikaanza kuisikia na muambatano wa sauti ya kike kwa mbali.
”..Samahani dada naomba kukuuliza kitu..?”
Alikuwa Mmama mwingine na ni  mgeni machoni mwangu kwani hata sikuwahi kumuona maishani mwangu. Sura yake pana iliyokuwa imeng’arishwa na manukato ya zile losheni zinazopendwa na baadhi ya kina dada wa uswahilini na waliokuwa na kipato kidogo. Zile  zinazojulikana sana kwa kubadilisha sura yako ya kutoka weusi nakuwa weupe. Wengi wanapenda kuiita ‘carolite’. Na kwa sasa harufu ile ya carolite ilikuwa inapambana na pua zangu zilizokuwa zimenasa harufu hiyo kali na inayochukiwa na baadhi ya wanaume wenye pesa zao. Niliendelea kumtolea macho huku nikijipa maswali mara mbili mbili ndani ya ubongo wangu nakuona sasa huyu huenda ndio akawa Mke wa mchungaji James kweli. Nilimkazia macho nakumjibu.
“..uliza tu mama yangu..?”
“..haya..! Ujue  nakufahamu sana binti japo wewe huwezi kunikumbuka mpaka nikukumbushe..?”
“..ni kweli unayosema mama..!”
Woga tayari ulishaninyemelea Tina mimi nakuona sasa haya ni majaribu haswa ya dunia. Nilikuwa mpole ghafla nakujidai mtakatifu tena Yule wa kanisani kabisa. Nilijinyenyekeza huku nikimtolea macho na kutega maskio yangu kwa kumsiliziza kwa umakini mkubwa.
“..nimekufuatilia muda mrefu.., kwanza kabisa pole na matatizo yaliokukuta kule tuliposafiri wote ikiwa ni pamoja na ajali tuliokuwa tumeipata..”
“..pole ya nini tena Mama. Mbona mimi sijasafiri nina muda mrefu nahii leo ndio kwanza nasafiri kuelekea Dar..?”
“..wala usitie shaka na mie. Mie nilikuwa mmoja wapo katika lile basi tulikuwa tumesafiri nalo jana kutoka Dar, na nakumbuka kabisa ulipandia kijiji fulani hivi japo kwa jina sikikumbuki na hapo ukapata siti tena kwa bahati nzuri ukakakaa na mchungaji mmoja hivi anaitwa mchungaji James..”
Akili yangu ikawa haitaki kabisa kukubaliaana na ukweli aliokuwa anaendelea kuongea huyu Mama. Sura yake kila nikiivutia kumbukumbu bado ilikuwa ni kazi kuikumbuka. Nilichokifanya niliendelea kumkana kama vile Yuda alivyomkana Yesu mara tatu..
“..wewe Mama utakuwa umenifananisha mie..?, embu niondokee hapa..!! Kwanza unavyoendelea kukaa na mimi, hiyo mikarolite yako inazidi kuharibu pua zangu..?”
Nilijifanya nimekasirika nakumgeuzia kibao yule Mama. Umati wa watu ukaanza kujaa katika eneo nililokuwa nimekaa na huyu Mama ukinizunguka. Yule Mama aligeuza macho yake huku na huku kana kwamba kafumaniwa ama ameona kitu cha ajabu sana kwangu.
“..nakupa dakika moja tu na wala siendelei.. Jibu ndio au hapana..?”
kwa muda huu yule mama alikuwa amebadilika sura na sauti nakuwa mbogo kwa muda. Kigugumizi cha ajabu kilichoambatana na kwikwi kali kikaanza kunishika Tina mimi huku nikiwa sina ujanja tena. Nikiwa bado najiandaa kumjibu yule Mama akanishika kwa nguvu ile blauzi yangu nakuanza kuropoka.
“..sasa utaeleza vizuri kwanini umemuua mchungaji wetu tena mchungaji James tuliokuwa tukimpenda sana kwa mahubiri yake..?”
Maskini Tina mimi nilijikuta nimeshaingia matatani tena, nilijitahidi japo kuzirudisha kumbukumbu kumtambua huyu Mama. Ndipo nikakumbuka kuwa jana wakati nipo safarini siti moja na marehemu mchungaji James aliniambia kuwa nilizimia mara mbili wakati ananiombea na tena wakisaidiana kuniombea na Mmama ambaye alikuwa mtu wa Mungu. Nilihuzunika sana nakuanza kuilaumu nafsi yangu kwa kutokufikiria. Nikiwa bado kwenye mawazo huku watu wakinishangaa mimi na huyu Mama. Mara huyu Mama akatoa sauti ya kuamuru kitu.
“.. jamani mapolisi binti mwenyewe ndio huyu hapa..!!, mchukuweni tumpeleke kituoni..”
Kumbe na mapolisi walikuwa wamenizunguka eneo lote nililokuwa nimezungukwa na watu ambapo walikuwa wamevalia nguo za kiraia. Walinichukuwa nakunipiga pingu huku umati wa watu ukinisikitikia kwa kitendo nilichokifanya cha kumuua mchungaji wao mchungaji James..





*** Inamaana ndio utakuwa mwisho wa safari ya Tina..?


*** Huyo Mama umeshamkumbuka..? na nini hatma ya Tina huko kituoni..?


*** Utamu wa story hii ndio kwanza unaanza kunoga. Endelea kufuatilia ujue ** Play gal – 55 itakuwaje..?



*****Itaendelea..*****
 

Labels:

1 Comments:

At July 28, 2012 at 12:02 PM , Anonymous Anonymous said...

aisee Andy unatisha uhondo ndo kwanza unaanza haya 2naendelea kusubiri.

 

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home