Monday, July 30, 2012

*** Play gal - 55 (Revenge)


Ilipoishia…

Nilihuzunika sana nakuanza kuilaumu nafsi yangu kwa kutokufikiria. Nikiwa bado kwenye mawazo huku watu wakinishangaa mimi na huyu Mama. Mara huyu Mama akatoa sauti ya kuamuru kitu.
“.. jamani mapolisi binti mwenyewe ndio huyu hapa..!!, mchukuweni tumpeleke kituoni..”
Kumbe na mapolisi walikuwa wamenizunguka eneo lote nililokuwa nimezungukwa na watu ambapo walikuwa wamevalia nguo za kiraia. Walinichukuwa nakunipiga pingu huku umati wa watu ukinisikitikia kwa kitendo nilichokifanya cha kumuua mchungaji wao mchungaji James..

Sasa endelea…

“..inuka twende hukoo..!!, husikii..?”
Machozi yangu hayakuwa mbali na uso wangu. Yalianza kunibubujika huku nikijifanya mbishi na king’ang’anizi wa kutokuinuka pale kwenye benchi. Ule umati wa watu ukazidi kuongezeka mara mbili yake nakuanza kupiga makelele ya kuwachochea wale mapolisi huku baadhi yao wakiangua vicheko vya hapa na pale. Sasa Tina mimi nikawa sina ujanja zaidi yakuendelea kushikilia benchi lile la kukalia wageni nikibakiwa na butwaa.
“..jamani, sio mimi niacheni..?, mmenifananisha jamani..?”
“..akufananishe nani mshenzi mkubwa wewe..? na leo ndio utaenda kuozea jela Malaya wewe..?”
Nilijikuta mwili wangu wote unakosa nguvu huku mapolisi wakinibeba juu juu kama vile mzoga wa mnyama tena mnyama mkubwa. Walinipiga kwa ubishi wangu wakugoma kunyanyuka kisha wakaniingiza ndani ya gari yao ya kipolisi huku ule umati wa watu pale stendi ukiwa pamoja nao kunisindikiza kwa makelele na vicheko na baadhi kuhuzunika na nadhani walikuwa wakimpenda sana mchungaji James.
“..kama kufa wacha nife leo leo tu..!  Sitapenda nikaozee jela angali bado kijana hivi..?”
Nilijisemea kwa sauti ya chini chini nikiwa ndani ya ile gari ndogo ya polisi huku baadhi ya polisi wakiwa wamenizunguka chini ya ulinzi mkali na mikono yangu ikishikamana vya kutosha na pingu. Zile nguo zangu zote nilizokuwa nimezivaa nilihisi kama zimelowa tena chapa chapa na si kwa maji bali kwa jasho na kojo lililokuwa likinitoka ovyo kwa woga wa hali ya juu likiendelea kupenyeza ndani ya nguo zangu zoote.
Kila mtu alikuwa akiendelea na shuguli zake. Hakukuwa na baridi sana na wala jua lilichelewa kutoka. Mawingu yaliendelea kuvutana nakuashiria dalili zote za kushuka kwa mvua lakini upepo mkali uliokuwa ukivuma kutoka mashariki kwenda magharibi ndio uliosababisha kukatisha mvua. Makaratasi pamoja na risiti za mabasi zote zilikuwa zimejaa mavumbi yaliosababisha na huu upepo uliojaa vumbi. Milango pamoja na madirisha navyo havikuwa mbali katika kupiga makelele. Kwa sasa macho yangu yalikuwa yamenitoka na niliangaza huku na huku ilikuvuta japo kumbukumbu kujua ni sehemu gani hapa nilipo. Nilijiangalia tena mara mbilimbili nguo zangu kama zimelowa lakini ndio kwanza zilikuwa kavu tena zilizojaa ubaridi.
“..Dada..?, basi limeshafika vipi huendi tena..? basi hilo hapo mbele yako limetokea Kigoma..”
Amani na furaha tele iliniingia ndani ya moyo wangu nakuanza kuamini kuwa kumbe vyote vile nilivyonitokea muda si mrefu haikuwa kweli bali ilikuwa ni ndoto. Eti mpaka mmama mmoja akanijia tena pamoja na mapolisi wakanichukuwa nakuacha umati wa watu ukipiga makelele kwa vicheko. Nilijisachi vizuri mifukoni mwangu kuangalia kama zile hela nilizochukuwa kwa mchungaji James bado zipo. Kwa bahati nzuri zote zilikuwepo. Nilitoa shilingi elfu thelathini nakumkabidhi konda kisha akanikatia tiketi ya kuelekea Dar es salaam.
Njia nzima hadi tunafika Singida bado nilikuwa sijiamini amini Tina mimi. Ndoto niliyokuwa nimeiota ilishanijenga tena vibaya ndani ya halmashauri ya ubongo wangu nakuona sasa nipo katika wakati mgumu. Sikutaka tena kufumba macho kwani niliamini nitaanza tena kuziota zilie zile ndoto mbaya na nitaumbuka humu kwenye basi Tina mie. Siti niliyopata ilikuwa ni ya dirishani na tena nilikuwa peke yangu kutokea Mwanza mpaka tulipofika Dodoma ndipo abiria mwingine akapanda na kukaa pembeni yangu. Alikuwa ni Mmama tu na tena alikuwa na mtoto mdogo anamyonyesha. Mwili wangu wote ukaanza kunisisimka kila nikimwangalia yule mtoto. Alikuwa ni mzuri sana kuanzia macho yake, masikio na hata mdomo wake. Kila mama yake alivyokuwa anambembeleza ndivyo na mie nilikuwa nazidi kusisimka mwili. Hisia kali zilinivuta mpaka nikakumbuka kwa jinsi nilivyoathirika na ukimwi na tena kuhusu kupata mtoto nisahau kabisa milele yote kama alivyoniambia dokta.
“…Jerry..?? Jerry..?? Kwanini Jerry umenifanyia hivi mie..?? Kwanini..?”
Taaratibu wimbi la matone ya machozi likaanza kunidondoka huku nikiendelea kumwangalia Yule mtoto. Ni Jerry ndio alioaharibu maisha yangu yote japo ni tamaa zangu za mwili ila amechangia kwa kiasi kikubwa kuniharibu kimaisha na kimasomo kwa ujumla. Kwanza yeye ndie alieniambukiza ukimwi. Pili ndio alionisababisha mpaka kwa hasira niache masomo nakuanza kudili na ndugu zake nao kuaambukiza.
“..alaaniwe Jerry huko alipo..!! Na ole wake nikifika Dar..?”
Nilijikuta uzalendo umenishinda nakuanza kuropoka ndani ya basi. Kitendo changu cha kuropoka japo kwa sauti ya chini chini kilinifanya nianze kujishtukia lakini kumbe hakukuwa na mtu yeyote aliyeniangalia ama kunishtukia. Hata yule mama ndio kwanza aliendelea kupekuwa pekuwa vitu vya mtoto wake vizuri nakuvipanga. Mwendo wa masaa matano na nusu tulikuwa tumeshapapita Morogoro na kwa muda huu tulikuwa tukiitafuta Chalinze. Akili yangu yote sasa nilikuwa nimeielekeza kwa Jerry ambaye ndio chanzo cha kuharibu maisha yangu kwa ujumla.
”..nitahakikisha nimemuua mmoja mmoja kama nilivyomuua mchungaji James..”
Niliongea kimoyo moyo huku nikiikaza sura yangu kwa hasira ya hali ya juu. Kwa muda huu yule mtoto mchanga aliyekuwa akilia alikuwa ameshapitiwa na usingizi mkali. Yule mama alikuwa kimya akijisomea kitabu  chake huku akihuziunika na kucheka hapo hapo kwa alichokuwa akikisoma.
“..mmhh kwa kweli hii hadithi ni nzuri sana sijawahi kuona..”
Alinigeukia nakuniongelesha huku akiwa kaendelea kushikilia kitabu kile cha hadithi.
“..kwani kikoje..”
“..kinaitwa ‘SITAKI TENA’  yaani hadithi ya humu ndani mhh..”
“..ikoje kama za shigongo..”
“..hapana hii ina muundo fulani hivi lakini inavutia na kuteka hisia zangu. Tangu nimeanza kuisoma nyumbani Dar es salaam bado sijaimaliza na haipiti muda naendelea kuisoma tena, nimekuja huku Dodoma njia nzima bado naendelea tu kuisoma na ndio kwanza bado kurasa kama arobaini ndio niimalize.
“..inaonekana ni ndefu eenhh..?”
“..anhh ndefu sana..!!, ni ‘novo’ kabisa hii. Yaani kuna binti humu ndani anaitwa Levina. Maskini amepata shida toka mdogo mpaka amekuwa bado anaishi katika mazingira magumu tu..”
Kuanzia Chalinze njia nzima ikawa ni yule mama ananihadithia ile hadithi ya Sitaki Tena. Nilianza kutekwa hisia zangu kwani baadhi ya matukio aliyokuwa amefanya yameendana na mimi kabisa.
“..enhee ikawaje sasa huyo Levina..”
“..yaani hadithi inavyoanza Levina akiwa bado mdogo sana anacheza rede na wenzake na kwa bahati mbaya na haraka haraka kimchezo, Levina anaokota jiwe nakumrushia mwenzake huku akidhania ni mpira. Basi lile jiwe linamfikia mwenzake kwa nguvu nakujikuta mwenzake akikata roho pale pale. Sasa hapo ndio hadithi inaanza sasa..”
“ennhh, nipe uhondo japo kidogo..”
“..mkasa unaanzia anapelekwa rumande. Huko mapolisi wa zamu wanambaka na kuharibu usichana wake. Kesi yake ilikuwa inasua sua kwani baba yake alipoteza nguvu ubavu mzima kwa mshtuko hivyo kitendo cha kufuatilia kesi kikawa chini ya mama yake na baadhi ya mawakili waliokuwa wanamsaidia. Mwisho wa siku levina akatumikia kifungo cha maisha gerezani..”
“..Mungu wangu..!!, ikawaje sasa..?”
“..hakukuwa na ujanja tena ikabidi asafilishwe mpaka kwenye gereza la watoto watukutu la mbeya amabapo ndipo maisha yake yakaanza upya..”
“..pliiz..!! pliiz..!!, nakuomba uniazime niendelee kupata uhondo halafu tukifika Dar es salaam nitakuachia, wewe si cha kwako,?..”
“..usijali..!!, chukuwa, endelea hapa nilipomaliza kukuhadithia..”
Akili yangu yote ikawa imebadilika vya kutosha. Mawazo yangu yote nikayahamishia kwenye hii hadithi ya ‘SITAKI TENA’ iliyokuwa imetungwa na mwandishi maarufu na ninayempendaga siku zote ‘ANDY RYN.’ Nilishawahi kusomaga hadithi zake kipindi cha nyuma facebook ila hii sijawahi kuisoma. Mwendo wa masaa mawili na nusu ulinitosha sana kuisoma hadithi robo nzima ya kile kitabu huku nikitamani kujua mbeleni. Sikuwa na ujanja tena kwani tulikuwa tumeshaingia ndani ya hili jiji la Dar es salaam. Giza lilikuwa limeshatanda muda mrefu tu kuashiria kuwa ni usiku japo sikufahamu ni usiku wa saa ngapi. Nilimkabidhi yule mama kitabu chake. Alikuwa na mizigo mingi chini ya basi hivyo akaniomba nimshikie mtoto wake na mkoba wakati wakushuka ili ahakikishe mizigo yake asije akaibiwa. Kwa upande wangu sikuwa na mzigo wowote hivyo nikamsaidia kubebelea mkoba wake na mtoto wake nikambeba kifuani kama mwanangu vile kisha nikaongozana na huyu mama kushuka.
Kitendo cha kutangulia kushuka yule mama akapokelewa na mwanaume huku akikumbatiwa. Halmashauri yangu ya kichwa ikafanya kazi haraka haraka nakutambua kuwa inawezekana akawa ndio mumewe. Sikumuona vizuri usoni kwa sasabu ya kukumbatiana na yule mama pia giza giza na mwanga ulikuwepo kidogo tena ile wa ndani ya basi japo kwa sauti zao ndizo ziliweza kupenyeza ndani ya ngome ya masikio yangu.
“..mwanangu Brayan yuko wapi..?”
“..Si huyo hapo amembeba huyo dada..?”
Aliongea yule mwanaume kwa sauti ya ukali naya nguvu akimuuliza mkewe huku akiacha kumkumbatia nakuangaza huku na kule ndipo jicho lake likakutana moja kwa moja na langu.
“…Tinaaa..? wewe si Tina wewe..?”
Alikuwa ni yule yule mvulana niliokuwa nikimchukia maishani mwangu na ndio yule aliyenipotezea malengo yangu ya kimaisha yote. Si mwingine bali alikuwa ni Jerry. Na kumbe huyu alikuwa ni mtoto wake. Nilijiuliza maswali mengi papo hapo japo sikupata jibu kwani ninavyokumbuka kuwa Jerry aliambiwa kuwa hawezi kumzalisha mwanamke kutokana na kwanza kuathirika na ukimwi na pili tulishawahi kumkata kata nanii yake na viwembe mimi na rafiki yangu Aisha na tulihakikisha tumeikata mirija yake yote inayopitisha mbegu za uzazi na hadi akazimia na kuwahishwa hospitali kipindi cha nyuma.
“..Tina mlete mwanangu nimesema..?”
Kwa sasa Jerry alikuwa amebadilika nakuwa mkali sana huku akinisogelea karibu. Mke wake alikuwa akimvuta kana kwamba aniachIe nakuwa mimi ni mtu mzuri tu tangu nimetoka naye safarini. Kila wakijibizana Jerry na mkewe ndipo na mimi nikapata nafasi ya kuwazunguka mpaka kwenye basi jingine nikalizunguka tena basi jingine nakuwatoroka pale pale pale huku nikiwa nimemshikiria mtoto wao.
“..ama nife mimi Tina..!, au Jerry..! sitamrudisha huyu motto kamwe..!!”
Nilijisemea kwa sauti ya chini chini huku nikitokomea mpaka kwenye geti la nje kabisa na nilipofika nje kabisa ndipo kwa mbaali nikasikia tangazo kuwa kuna dada ametoroka na mtoto na amevaa suruali ya jinsi akiwa na mkoba mweupe. Eti akamatwe popote alipo humu ndani ya stendi..
“..It’s too late Jerry..!! (Jerry umeshachelewa..!!)”
Niliongea kwa kujidai huku nikipanda dalaladala yakuelekea Mbagala na nisijue naenda kwa nani na wala itakuwaje huko nieandapo na huyu mtoto..






*** Unavyodhani Tina atakamatwa na Jerry..? Kwanini Tina kaamua hivyo kufanya..?


*** Nini hatma ya Tina kama akikamatwa na Jerry..?


** Hii ndio Play gal (Revenge) , Usithubutu hata kidogo uhadithiwe inayoendelea kwani play gal 56 itakayofuata ni nzuri zaidi ya hapa..



****Itaendelea…****

Labels:

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home