Sunday, July 8, 2012

Maelewano katika Mahusiano..



Mahusiano ni kama mchanga uliowekwa katika kiganja cha mkono wako, utakapoushika vizuri na wazi, mchanga huo utabakia kuwa katika kiganja. Pale utakapojaribu kufunga mkono, kuminya na kubana kwa nguvu mkono wako ili kuuzuia mchanga huo, basi bila shaka utaanza kupenya katikati ya vidole vyako na kumwagika chini. Utaweza kuuzuia kiasi utakapoanza kumwagika, lakini mwingi utaishia chini. Mahusiano ndivyo yalivyo.
Yakupasa kumkubali mwenzako kwa nia njema na malengo yaliyo wazi ili kuweka maelewano ya pamoja kati yenu, na kwa namna hiyo mahusiano yenu yatashamiri. Mahusiano yakiachwa kuwa wazi lakini kwa kuheshimiana na uhuru baina ya wawili ni rahisi kuendelea kuwa imara. Lakini yanapobanwa ama mmoja wapo kumtawala mwenzie na kuwa na mamlaka zaidi, mahusiano hayo yataponyoka, kuyayuka na hatimae kupotea.

Mahusiano mengi ambayo yanashindikana na hatimaye kuelekea kuvunjika, talaka na kuachana hutokana na sababu kubwa ni : baada ya muda fulani katika mahusiano, mawasiliano yanapungua baina ya wawili hao, kutokuelewana kunajitokeza na maelewano katika mambo ya msingi yanatoweka!
Sababu nyingine kubwa ambayo inapelekea kuvunjika kwa mahusiano ni kutopeana muda wa kutosha kuwa pamoja kama wapenzi, katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi kujitolea muda kuwa pamoja na mwenzako, familia ama ndugu imekuwa ni tatizo kubwa.
Tatizo kubwa zaidi katika mahusiano linakuja hasa kutokana na sababu watu wengi wanajiingiza katika mahusiano ili kupata kitu fulani: wanajaribu kupata mtu ambaye atawafanya wajisikie vizuri.
Ukweli ni kwamba , namna pekee ambayo unaweza kupangilia mahusiano yako yaweze kudumu na kushamiri ni kuwa tayari kujitolea zaidi kuliko kutegemea kuwa mpokeaji tu katika mahusiano yenu!
Talaka na kutengana katika mahusiano huacha madhara makubwa sana kwa wahusika hasa kwa upande wa afya zao; usumbufu wa akili hutokea, na matatizo kama midhaiko na ukosefu wa amani. Kumukumbu za mahusiano yaliyopita hukuandama na kusababisha kujishushia heshima, kutokujiamini na mambo mengine kama hayo.
Ni vigumu sana kupita katika matatizo kama hayo na kuweza kuhimili hali kama hizi baada ya kutokea. Hutokea hali ya kutojiamini tena na kuogopa kuingia katika mahusiano mengine ama kukurupuka na kujiingiza katika mahusiano mbalimbali bila kutafakari. Mara nyingi uwezo wa kufikiri na hata wa kufanya kazi wa watu waliokumbwa na matatizo kama haya hupungua, na hubadilika toka kuwa yenye kujenga zaidi na kuwa ya kubomoa zaidi kwa maisha binafsi ya wahusika. Madhara haya hutokea katika mazingira amabayo muhusika anapambana kujiweka katika hali ambayo atajisikia kila kitu kiko sawa kwa upande wake, wakati inakuwa sivyo.

Jambo ambalo linasababisha UELEWA/ MAELEWANO kuwa jambo gumu zaidi ni kuwa yatupasa zaidi kusikiliza na kuelewa nafasi ya upande wa pili wa wenzetu ambao tuna mitazamo tofauti. Hatupaswi kukubaliana nao, lakini hatuna budi kuwasikiliza. Labda, kutokana na ustaarabu yanaweza kutokea maelewano ya pamoja namna gani kila mmoja ameelewa namna mwenzake anavyochukulia na kuamini katika jambo husika… hata kama mwisho wa siku mtakuwa hamkubaliani kati yenu bado.
Hivyo, kabla hujakumbwa na bahati mbaya ya kujiingiza katika mahusiano yatakayoishia kuvunjika ama talaka, chukua tahadhari kumwelewa na kuelewana na mpenzi wako vizuri zaidi, ni vyema kila mmoja akajua uwezo na udhaifu wa mwenzi wake na namna gani anaweza kukabiliana na mapungufu yatakayojitokeza.
Jumapili njema...

Labels:

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home