Thursday, August 16, 2012

HATUA ZA KUMRUDISHA MPENZI WAKO ULIOACHANA / KUGOMBANA NAYE..


Karibuni sana wapendwa katika blog yetu hii ya bongomixx. leo ningependa tuzungumzie jisi ya kumrudisha mpenzi ambaye umeachana naye ama yupo mbali na wewe ama umepoteana naye kwa muda mrefu.
Kugombana ni sehemu ya maisha ya binadamu. Yawezekana kabisa ulikuwa na mwenzi wako ambaye ulimpenda kwa moyo wako wote na sasa mmeachana. Kutengana kuna mambo mengi, wakati mwingine ilikuwa hasira tu.
Siku zote baada ya hasira kuisha, moyo hubaki peke yake katika nafasi yake halisi ya kufanya maamuzi. Hapo ndipo kwenye lengo la mada yetu ya leo. Kwamba kwa msingi huo umegundua kwamba kumbe mpenzi wako uliyeachana naye, bado unampenda.
Kwamba hata makosa aliyokuwa akiyafanya, ulimsababishia au si makubwa kiasi cha kuachana na badala yake mnaweza kukaaa na kuzungumza kiutu uzima na kuyamaliza. Yes! Hilo ndilo ninalotaka kulizungumzia.
 
Upo tayari rafiki? Je, uko katika kundi hilo? Unataka kumrudisha mpenzi wako wa zamani? Kama majibu ni ndiyo, mada hii inakuhusu sana.

JE, NI SAHIHI?
Baadhi ya watu huamini kwamba kurudi kwa mara nyingine kwa mpenzi wa zamani ni kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha. Kwamba hakuna mwanaume wala mwanamke mwingine yeyote atakayeweza kuwa naye tofauti na huyo anayemrudia.
Jambo hilo si la kweli hata kidogo, kikubwa cha kuzingatia hapa ni moyo; je, unahisi bado unampenda? Ni kweli naye anakupenda? Kama sifa hizi zipo, hayo mambo madogo ambayo mmetofautiana ni ya kawaida kabisa ambayo mnaweza kurekebishana taratibu.
Kwa msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika kurudiana na mpenzi wako wa zamani, maana tayari unakuwa umeshamjua vya kutosha, hivyo kukupa urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na kuepuka asiyopenda jambo litakalozidisha umri wa uhusiano wenu, si ajabu mkaingia kwenye ndoa.

UTAFAIDIKA NA NINI?
Utafiti usio rasmi nilioufanya, unaonesha kwamba zipo faida za kurudiana na mpenzi mliyeachana, lakini kikubwa ni awe moyoni mwako.
Hebu msikie Julius Kihesupe wa Uwanja wa Ndege, jijini Dar es Salaam, ambaye alipata kuzungumza nami hivi karibuni akitoa maoni yake kuhusu suala hili: “Si vibaya kurudiana, maana kwanza mnakomaza uhusiano.
“Kumrudia mtu wako wa zamani maana yake ni kwamba umekubaliana na udhaifu wake wote. Unajua anachopenda na anachochukia, hapo lazima mtadumu. Bila kudanganya, mke wangu wakati wa urafiki wetu, tukiwa na miaka miwili kwenye uhusiano tulitibuana tukaachana.
“Kila mmoja alikaa kivyake kwa miezi kama sita hivi, nikakutana naye Dar, nikiwa nimeachana naye Mbeya, nikamwita tukakaa na kuzungumza, miezi minne mbele yake tukafunga ndoa.”

CHUNGUZA ALIPO
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kuchunguza ni mahali anapopatikana kwa wakati huo, nasema hivyo kwa sababu yawezekana alihama makazi, kikazi n.k. Kujua anapopatikana ni mwanzo wa kuelekea kwenye mafanikio ya kumkamata katika himaya yako.

ANA HISTORIA GANI?
Lazima ujue kuhusu historia yake kiuhusiano baada ya kuachana na wewe. Hapo unatakiwa kufanya ‘ushushushu’ wako kimyakimya bila yeye kujua. Ikiwa ameshafanya ‘vurugu’ sana, maana yake ni mtu asiye na msimamo na huenda anaongozwa zaidi na tamaa za kimwili na si mapenzi.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana kujua kama muda huo ambao wewe unahitaji kurudi tena mikononi mwake kama ana uhusiano mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya uhusiano, itakubidi uhairishe zoezi lako.
Unatakiwa kufanya hivyo kwa sababu kwanza, anaweza kukubali kuwa na wewe wakati akiwa bado hajaachana na mpenzi aliyenaye kwa muda huo, hivyo kuwa kama mwizi tu kwa mwenzako.
Kubwa zaidi ni kwamba, utakuwa katika mapenzi ya kushea, jambo ambalo si zuri kisaikolojia na hata kiafya.

Kumbuka kwamba, unaweza kuwa na mwenzi wako, mkapendana kwa dhati na mkadumu kwa muda mrefu, lakini kwa bahati mbaya mkaachana kwa sababu ambazo mnazifahamu wenyewe.
Katika muda mfupi ambao utakuwa umeachana naye, anaweza kufanya mambo ya ajabu sana. Pamoja na kwamba moyo wako unamhitaji, lakini anaweza kuwa tayari ameshapoteza sifa za kuwa na wewe. Katika hali hiyo, ni sahihi kurudiana naye? Bila shaka jibu hapa ni siyo sahihi.
Wiki iliyopita tulianza kuangalia kama ni sahihi kurudi kwa mwenzi huyo, faida utakazopata kwa kurudiana naye, kuchunguza sehemu anayopatikana na kufuatilia historia yake baada ya kutengana kwenu.
Enheee! Sasa twende kwenye vipengele vingine.



MAWASILIANO

Ukishachunguza mahali alipo na kuridhika na historia yake ya kimapenzi baada ya kuachana na wewe, sasa unatakiwa kutafuta mawasiliano yake. Kupata mawasiliano yake ni hatua ya kwanza, kitakachofuata baada ya hapo ni kujenga mawasiliano. Hapo sasa inategemea na namna mlivyoachana, lakini kama hamkuwa na ugomvi mkubwa sana, basi unaweza kumtumia meseji za kichokozi mara nyingi uwezavyo kwa siku.Majibu yake ndiyo yatakayokupa mwanga wa kuendelea na kipengele kingine. Kikubwa hapa ni kutozungumzia kabisa mambo ya mapenzi, badala yake iwe ni kumjulia hali na utani wa hapa na pale.



MPE MWALIKO


Baada ya kutengeneza mawasiliano naye, sasa unatakiwa kumwalika katika shughuli mbalimbali za kifamilia na binafsi. Mathalani umepata mwaliko wa kwenda kwenye sherehe au hafla fupi ya usiku, omba kampani yake.
Kama mtu mzima atagundua kitu kilichopo moyoni mwako. Hata kama atakuwa mwenye moyo wenye kutu, kutoka naye mbele za watu, kutamfanya akumbuke enzi zenu mlipokuwa mkitoka pamoja, hivyo kufikiria kurudi tena kwako.Ikiwa ataamua kukuambia kwamba anaona mrudiane litakuwa jambo zuri zaidi, maana atakuwa amekurahisishia, lakini akinyamaza, basi njia inayofuata hapa chini ni muafaka kwake.



MVUTE KARIBU YAKO

Sasa unatakiwa kumsogeza karibu zaidi na wewe. Lazima afahamu kwamba, kuna kitu fulani kipo ndani ya moyo wako. Meseji zako zibadilike, kama ulikuwa unamwandikia, “Vp uko poa?” au “Mambo yanaendaje?”, sasa unatakiwa kubadilisha hadi “Niambie sweetie, uko poa?”Meseji za aina hiyo zitamfanya aone tofauti na inawezekana kabisa akagundua kwamba upo kwenye mawindo ya kumrudisha tena kwako. Katika hatua hii katu hutakiwi kufungua mdomo wako kumwambia kuwa unataka kurudiana naye na badala yake unatakiwa kuacha vitendo vizungumze vyenyewe.

OUTING
Kutokana na ukaribu wenu, kumwalika katika mtoko wa chakula cha mchana au usiku, haitakuwa vigumu kwake. Hiyo itakuwa njia nyingine ya kumfanya awe karibu yako zaidi.Mkiwa katika mtoko huna haja ya kuzungumza chochote kuhusu uhusiano wenu, labda kama yeye ataanzisha mjadala huo. Ongelea mambo mengine ambayo ni maarufu zaidi labda katika duru za siasa, sanaa n.k lakini si mambo yanayohusu mapenzi kabisa.Kama kichwani mwake alikuwa amekufanya kama rafiki yake wa kawaida, mtazamo utaanza kubadilika taratibu na kuanza kutamani kurudi tena mikononi mwako. Jaribu kufikiria, kama umetoka naye, akiamini labda unataka kumuomba msamaha na kurudiana naye, wewe unaanza stori za soka! Bila shaka atajiona kama mpumbavu kichwani, si ajabu akaamua kujifunga mwenyewe kwa kuomba urudi tena kwake.



JADILI PENZI LENU
Hatua hii ndiyo muhimu zaidi hapa; sasa unatakiwa kuanza kuzungumzia juu ya uhusiano wenu. Mwambie jinsi ulivyokuwa ukifurahishwa na mapenzi yenu. Msifie alivyokuwa anajua majukumu yake na kukuonesha mapenzi ya dhati.Si vibaya kama utamweleza pia sababu ambazo unahisi zilisababisha wewe na yeye kuachana. Kwa kauli hizo utampa nafasi ya kuchambua/kumjua mwenye makosa na mahali pa kurekebisha.


KIRI MAKOSA YAKO
kiwa kuna mahali unaamini ulikwenda kinyume na yamkini ndiyo sababu kuu iliyosababisha muachane, kiri makosa yako mbele yake. Mweleze kwamba wewe ndiyo chanzo cha matatizo na huenda kama si kukosea, msingeachana.Kujutia hasa kama uso wako utawakilisha vyema kilicho moyoni mwako, kutamfanya akuone muungwana ambaye unatambua ulipojikwaa na sasa unataka kurekebisha makosa yako. Hapo utakuwa na nafasi kubwa ya kumnasa kwa mara nyingine.


MWELEZE YAKO YA MOYONI
Sasa huna sababu ya kuendelea kujitesa, toa dukuduku lako. Mwambie moja kwa moja kilichopo moyoni mwako. Kwamba unahitaji nafasi nyingine kwake, maana umeshajua makosa yako.
Hii ni nafasi ambayo si rahisi kabisa kuchomoka. Itumie vilivyo. Sauti yako pekee itoshe kumaanisha kile kilichopo moyoni mwako. Lazima atakuelewa.
Kama utakuwa umefuata kwa makini vipengele vyote hapo juu, lazima urudi tena mikononi mwake. Kuna nini tena? Ameshakuwa wako huyo, ila kuwa makini usimpoteze tena.

AKIKATAA JE?
Pamoja na kufuata vipengele vyote hivyo, inawezekana akakataa. Kukataa kwake lazima kuna sababu nyingi. Mwingine anaweza kukuambia moja kwa moja sababu za kukataa kurudiana na wewe wakati mwingine anaweza asiseme chochote.
Huenda akakumbia kwamba tayari ana mtu wake, au hafikirii kurudi mikononi mwako; usihuzunike.
Ni bora sana huyu anayekuambia ukweli, kuliko kurudi halafu ukutane na mateso yale yale.Inawezekana labda hana mapenzi na wewe. Kama ndivyo, kuna sababu gani ya kujikomba? Kubaliana na ukweli, halafu subiri mwingine!
Sikia, subiri mwingine na siyo utafute, maana mwenzi wa kweli huja mwenyewe, hatafutwi!

Labels: ,

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home