Habari Leo jumatatu wapendwa wa blog yetu ya bongomixx.
MAAJABU yametokea kwa msichana mkazi wa kijiji cha Mpasa
mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa, kujifungua mtoto asiye
wa kawaida baada ya ujauzito wa zaidi ya miaka mitatu
Mtoto aliyekuwa kivutio na gumzo kijijini hapo na
kwingineko, alizaliwa Agosti mosi, akiwa na meno 32 ambayo ni idadi ya mtu
mzima na nywele zenye mvi utosini huku mzazi Lucia Sabastiano (18) akidai kuwa
hakuwahi kukutana kimwili na mwanamume yeyote maishani mwake.
Mtoto huyo ambaye alifariki dunia baada ya siku mbili,
alikuwa wa kiume, huku pia akiwa na sehemu za siri zilizokomaa kama za mtu
mzima ambazo zilikuwa na nywele ndefu sehemu hizo.
Maumbile mengine ambayo yalionekana kuwa ya ajabu ni
pamoja na midomo kuwa myekundu, mikono na miguu yenye kucha ndefu na viungo
vingine vikionekana sawa na vya mtu mzima.
Akizungumzia tukio hilo jana, Ofisa Mtendaji wa Kijiji
cha Mpasa, Privatous Maliyatabu alisema msichana huyo ambaye alipata ujauzito
huo akiwa mwanafunzi wa darasa la tano, alijifungua saa 10 alasiri nyumbani kwa
mjomba wake aliyetajwa kwa jina moja la Mwelela.
Maliyatabu alisema Lucia alijifungua kwa msaada wa
mkunga wa jadi aliyejulikana pia kwa jina moja la Mama Pashaa, baada ya kupewa
dawa ya kunywa na mganga wa jadi, Maneti Mazimba.
Kwa mujibu wa Lucia, licha ya kupata ujauzito huo, bila
kukutana kimwili na mwanamume maishani mwake, alidai kutojua jinsi alivyopata
ujauzito huo na kudumu nao miaka mitatu.
“Nakumbuka siku moja nilisimama mlangoni mwa nyumba yetu
na ghafla nikaona kama mwujiza, mwanga mkali mbele yangu na kisha kujitokeza
sura ya mwanaume ambaye siwezi kuhadithia umbile lake na akatoweka na tangu
hapo, nilianza kuhisi tumbo kujaa na kuhisi kiumbe kikicheza,” alidai Lucia.
Baadaye aliwaeleza wazazi wake ambao walimpeleka
hospitali baada ya kuona tumbo lake linaongezeka siku hadi siku, lakini kwa
nyakati tofauti Lucia alipimwa katika hospitali tofauti na kuambiwa hakuwa na
ujauzito.
Alisema:“Kila waliponipima waliniambia kuwa sina mimba,
lakini miye nilikuwa nikihisi kitu kama mtoto kinacheza tumboni kwa kipindi
chote cha miaka mitatu, hali hiyo ilizidi kunishangaza.
Mmoja wa ndugu wa Lucia ambaye hakutaka jina lake
litajwe, alisema wana uhakika ndugu yao hajawahi kukutana na mwanamume maishani
mwake na familia nzima ilishangazwa na ujauzito wake.
“Lucia ni miongoni mwa watoto watatu katika tumbo la
mama yetu, na amekuwa akitushangaza kwa yaliyokuwa yakimtokea tangu apate
ujauzito huu, kwani mara nyingi usiku amekuwa akiweweseka, hali iliyofanya
tuanze kuhangaika naye kwa waganga wa jadi baada ya hospitali kutueleza kuwa
hana kitu tumboni,” alisema mwanandugu huyo aliyejitambulisha kuwa ni dada
yake.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Emmanuel Mtika
alisema kitaalamu ujauzito unatakiwa kuwa kati ya wiki 38 na 40 na ikizidi sana
wiki 42 hadi kujifungua na kuongeza kuwa hakuna ujauzito wa miaka mitatu.
“Inawezekana huyu mwanamke alikuwa na matatizo ya uvimbe
tumboni kwa muda mrefu na akapata ujauzito wa muda wa kawaida ihali yeye
akiamini kuwa alikuwa mjamzito kwa kipindi kirefu kumbe sivyo,” alisema Dk
Mtika.
Alisema kinachoshangaza ni maelezo ya kudai kuwa
mjamzito bila kukutana na mwanamume, kwani hakuna mwanamke anayeweza kupata
ujauzito kwa hali hiyo.
“Inawezekana kuna mwanamume alitaka kufanya naye mapenzi
kwa nguvu, lakini hakufikia sehemu mwafaka na labda mbegu za kiume zilimwagika
karibu na sehemu zake za siri na kumwingia, hapo uwezekano wa kupata ujauzito
upo,” alisema Daktari.
Hata hivyo, Dk Mtika alisema mwanamke huyo hakwenda
hospitali kubwa kupata vipimo ili kubaini tatizo lililokuwa likimsumbua kwa
kipindi chote hicho.
Labels: ~ Tambua ~, news updates
0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home