Sunday, July 8, 2012

Mawasiliano katika Mahusiano...



Leo katika tasfiri zetu nitaanza na tafsiri ya Umuhimu wa Mawasiliano katika mahusiano ambao ni msingi mkuu katika misingi mitano ya mahusiano ama ndoa bora.
Mawasiliano mazuri katika mahusiano ni moja ya suala muhimu sana linaloweza kusaidia mahusiano yenu yawe na mafanikio.

Siyo kila mtu anajua namna bora na makini ya kuwasiliana kwa kuzaliwa nayo, hata hivyo tunaweza kujifunza. Basi kama una matatizo ya mawasiliano mazuri katika mahusiano yako unaweza kujifunza kwa kusoma makala hii.
Ukijifunza mbinu za kuwasiliana kila inapobidi na kwa namna inayotakiwa utaweza kusaidia mahusiano yako kuwa bora na yenye furaha na kuepuka kubaki katika mashaka ya ndoa yako kuingia katika orodha ya ndoa zilizovunjika.
Mawasiliano hayana maana ya kuongea tu. Kipengele muhimu sana katika mawasiliano ni uwezo wa kuwa msikivu. Wakati mwingine ni hilo tu linahitajika, kusikiliza tu!
Mwenzako anaweza akawa anahitaji kusikilizwa tu ili kuweza kutatua tatizo ama kuondoa mashaka yaliyokuwapo. Kama utahitajika kujibu ama kuelezea kuhusu jambo fulani basi baada ya kumsikiliza mwenzako kwa umakini mkubwa wote wawili kwa pamoja mnapaswa kujaribu kujadiliana na kufikia muafaka wa tatizo husika.
Mawasiliano ni suala pana kwa ujumla, ni pamoja na maneno ya kutamkwa na mambo ambayo si ya kutamkwa-matendo ama ishara. Mbinu za mawasiliano makini katika mahusiano zinajumuisha namna zote mbili za kuwasiliana na kuziainisha kwa uhakika.

Tuchukue mfano, kama mpenzi ana hasira, anaweza akakaa amefumbata mikono kimya akikutizama tu bila kusema neno. Hali kama hiyo ni jambo ambalo linahitaji umakini wako wa haraka. Kama utanyamaza na kumwacha bila ya kufanya chochote utasababisha ajisikie kususwa, kutohitajika na kupelekea mambo kuwa mabaya zaidi. Kusoma sura na matendo ya mwenzako ni kipaji ambacho unapaswa kufanyia kazi vyema. Kinakuwezesha kuelewa mambo mengi sana kuhusu mwenzako anavyojisikia kwa wakati fulani na kugundua hata kama anadanganya.

Kama wewe ni mtu makini na mwerevu basi unaweza kugundua mbinu mbalimbali za mawasiliano makini kwa kutilia maanani tu mambo yanayoendelea katika mazingira uliyopo. Ni vyema kama unahitaji msaada zaidi ili kuelewa mbinu mbalimbali za mawasiliano mazuri ukahudhuria mafunzo maalumu au kusoma vitabu mbalimbali kuhusu jambo hilo. Hii inaweza ikakugharimu kidogo lakini thamani yake itakuwa kama dhahabu pale ambapo itaweza kukusaidia kuokoa ndoa ama mahusiano yako.

Mawasiliano mazuri ni pamoja na kutoa kipaumbele hata kwa mambo madogo madogo na kumwonyesha mwenzako kwamba anathaminiwa. Kumwambia asante mpenzi wako isiwe ni jambo gumu. Kuonyesha kuridhishwa na jambo fulani ni ukarimu wa kawaida katika maisha.

Usichoke ama kukata tamaa kutamka, “NAKUPENDA”, ama “ASANTE” au “POLE” ama muhimu zaidi "SAMAHANI". Maneno haya ni vyema yakawa sehemu muhimu sana ya mahusiano yenu. Kila mtu anahitaji kujisikia anathaminiwa.

Uelewa ama maelewano ni sehemu nyingine muhimu katika mawasiliano ambayo imeachwa bila kufanyiwa kazi. Tukisema bila kufanyiwa kazi ina maanaisha kwamba mara nyingi katika mazingira mbalimbali ya mahusiano, hayaulizwi maswali ya kutosha kuweza kuweka mambo bayana. Tunadhania kwamba tunajua kile ambacho wenzetu wanakiongelea bila kutaka kueleweshwa vizuri zaidi. Kudhania mara nyingi kutakupeleka katika matatizo. Hivyo hakikisha unaelewa kwa uhakika ni nini kinaongelewa. Kama huelewi, uliza maswali hadi pale kila kitu kitakapokuwa wazi na kueleweka.

Ushauri bora kwa suala hili ni kujifunza, kujaribu, kujaribu na kujaribu. Jifunze mbinu za mawasiliano bora na makini katika mahusiano na kufanyia majaribio kila siku. Baada ya muda yatakuwa kama asili yako na hutapata tabu tena ya kufikiria namna ya kuwasiliana.

Kumbuka, bila juhudi na kujitolea kuwa na mawasiliano makini na bora katika mahusiano, mahusiano hayo ni sawa na mahusiano-mfu!

Anza sasa kuwasiliana ipasavyo… na jenga mahusiano/ndoa bora!

Labels: ,

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home